eeas.europa.eu

Ulaya Yaleta Mabadiliko kwa Wakulima wa Tanzania

Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, kikiajiri zaidi ya asilimia 65 ya wananchi na kuchangia takribani asilimia 30 ya Pato la Taifa (GDP). Hata hivyo, kwa miongo mingi, wakulima wadogo—ambao ndio moyo wa sekta hii—wamekumbana na changamoto kubwa. Katika hii makala, Balozi wa EU, Christine Grau, anaangazia jinsi **AGRICONNECT**, programu kubwa ya kilimo iliyofadhiiwa na EU katikasekta ya kilimo nchini Tanzania, imeleta mabadiliko chanya.

**Na** _**Christine Grau Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki.**_

Kiwanda cha kusindika mbogamboga, matunda na viungo cha Mbeya (Mbeya Food Park) kilikuwa eneo sahihi kuhitimisha AGRI-CONNECT, programu kabambe ya kilimo iliyofadhiliwa na Umoja wa Ulaya katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania na Zanzibar. Kiwanda hiki cha kisasa kimeimarisha kwa kiasi kikubwa usindikaji wa mazao na upatikanaji wa masoko kwa biashara ndogondogo. 

Kabla ya kuanzishwa kwake, wazalishaji wadogo na wajasiriamali wa kilimo walikabiliwa na changamoto za kufikia masoko, kuboresha ubora wa bidhaa, na kupata mtaji. Leo, wanasimama kama ushahidi wa kile ambacho fursa, uwekezaji, na msaada sahihi vinaweza kuleta matokeo chanya.

Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, kikiajiri zaidi ya asilimia 65 ya wananchi na kuchangia takribani asilimia 30 ya Pato la Taifa (GDP). Hata hivyo, kwa miongo mingi, wakulima wadogo—ambao ndio moyo wa sekta hii—wamekumbana na changamoto kubwa. Mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa fedha, miundombinu duni, na ukosefu wa masoko vimepunguza uwezo wao wa kuzalisha na kuuza mazao yao kwa faida.

Ndiyo maana Umoja wa Ulaya umeipa kilimo kipaumbele, ukiwekeza TZS bilioni 270 (€100 milioni) kupitia AGRI-CONNECT ili kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya kilimo, kuboresha barabara za vijijini, na kukuza lishe bora.

Lakini AGRI-CONNECT haukuwa tu mpango wa kifedha; ulikuwa pia uwekezaji katika maisha ya watu. Mfano bora wa mafanikio haya ni safari ya Bertha Mwaipopo na kampuni yake, _Libeta Products_. Alipoanza biashara yake ndogo ya kusindika viungo, alikuwa akifanya kazi kutoka jikoni kwake katika nyumba ya chumba kimoja, bila ujuzi wa matumizi mazuri ya fedha au uuzaji. 

Usafirishaji ulikuwa mgumu, na kuhifadhi bidhaa ilikuwa changamoto. Miaka michache baadaye, ameipanua biashara yake, akiuza bidhaa katika mikoa zaidi ya mitano na kuwaajiri wanawake 15. Mafunzo, ushauri, na upatikanaji wa vifaa vya kisasa kupitia Kiwanda cha Mbeya Food Park—rasilimali zilizowezeshwa na AGRI-CONNECT—vilimpa mwanga mpya wa kibiashara.

Kiwanda hiki cha Mbeya Food Park, kilichoko Barabara ya Uwanja wa Ndege wa Zamani jijini Mbeya, ni moja ya miradi ya kudumu ya programu hii. Hiki kiwanda kimewapatia wajasiriamali wadogo mashine za kisasa, maghala ya kuhifadhi bidhaa, na mafunzo ya kuboresha bidhaa zao. Kimesaidia kubadilisha namna ya usindikaji wa chakula, hasa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ikichangia biashara kukua na kushindana katika masoko makubwa na yenye wigo mpana zaidi.

Lakini faida za program hii hazikuishia kwenye biashara za kilimo pekee.

Katika safari yangu kuelekea Mbeya kutoka Dodoma, nilisimama katika soko kuu la Iringa na kuona mazao mbalimbali—matunda, viungo, na nafaka—yenye uhitaji wa minyororo imara ya thamani ili kuyasindika na kuyapakia kwa ubora wa hali ya juu. Kama ilivyo Mbeya, mkoa wa Iringa pia umenufaika sana na AGRI-CONNECT, huku wakulima wakipata barabara bora, vifaa vya usindikaji, na msaada wa kibiashara.

Baada ya tukio la kufunga programu hii, tulisafiri kilomita 30 kupitia vilima vya wilaya ya Rungwe. Ilikuwa safari inayokufanya utambue kwa nini kilimo ni muhimu—si tu kama sekta muhimu ya kiuchumi, bali kama sehemu ya msingi ya maisha ya watu. 

Tulifika Rugwe kuzindua barabara mpya ya: _Masebe Dispensary – Mpuguso TTC – Kibaoni_, ambayo ni sehemu ya kilomita 5 kati ya zaidi ya kilomita 160 za barabara za vijijini zilizoboreshwa kupitia AGRI-CONNECT. Barabara hizi nazichukulia kama mashujaa wasioonekana wa ukuaji wa kilimo. Bila barabara bora, hata mavuno mazuri zaidi yanaweza kuoza kabla ya kufika sokoni. Wakulima wa Nyanda za Juu Kusini—zaidi ya 177,000—sasa wanapata njia bora, salama, na za haraka za kusafirisha mazao yao.

Pamoja na hayo, zaidi ya ajira 516,000 zimezalishwa kupitia AGRI-CONNECT. Miradi ya miundombinu 166 imekamilika. Vituo 85 vipya vya usindikaji vimeanzishwa, na kampeni za lishe bora zimewafikia asilimia 63 ya Watanzania.

Haya ni mafanikio ambayo yanaonekana moja kwa moja katika maisha ya watu—biashara zinazostawi, wakulima wanaounganishwa na masoko, na jamii zinazopata lishe bora.

Ingawa programu ya AGRI-CONNECT imefikia tamati, mchango wa Umoja wa Ulaya katika sekta ya kilimo Tanzania bado utaendelea. Kupitia mpango wa _Global Gateway_, tutaendelea kuwekeza katika minyororo ya thamani, kuboresha miundombinu ya usafirishaji, na kupanua fursa kwa wakulima wadogo. Kwetu tunachukulia AGRI-CONNECT kama hatua katika safari ndefu ya kuifanya sekta ya kilimo kuwa thabiti zaidi, shindani, na endelevu.

Tulipokuwa tukirejea kutoka Rungwe, mafanikio yaliyopatikana yalionekana dhahiri kupitia barabara tulizosafiri, biashara tulizotembelea, na wakulima tuliokutana nao. Vyote hivi vilitukumbusha kuwa tukiwekeza sawa, tunajenga misingi na mabadiliko ya ukweli yanayodumu katika sekta ya kilimo haswa katika sekta za chai, kahawa na mboga mboga. Mafanikio halisi ya AGRI-CONNECT hayataonekana tu katika ripoti au jedwali la takwimu, bali katika maisha ya watu waliyonufaika hususan kwa wakulima wa Tanzania.

_Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la_ [_Habari Leo_](https://habarileo.co.tz/ulaya-yaleta-mabadiliko-wakulima-tanzania/) _tarehe 24 Machi 2025._

Read full news in source page